Omanyala afanya mazoezi nchini Ufaransa kabla ya Rabat Diamond League – Taifa Leo


Omanyala afanya mazoezi nchini Ufaransa kabla ya Rabat Diamond League

Omanyala afanya mazoezi nchini Ufaransa kabla ya Rabat Diamond League

Na GEOFFREY ANENE

MTIMKAJI Ferdinand Omanyala yuko mjini Miramas, Ufaransa kwa mazoezi kabla ya kuanza kampeni yake ya riadha za Diamond League mjini Rabat, Morocco mnamo Mei 28.

Omanyala alishinda mbio za ukumbini za Assembly de Miramas katika mita 60 mwezi Februari 2022 na kukamata nambari mbili Februari 2023.

Vyombo vya habari vya Ufaransa vimesema Alhamisi kuwa afisa huyo wa polisi amerejea Miramas kwa matayarisho.

Omanyala, ambaye ni bingwa wa Afrika na Jumuiya ya Madola, anajivunia rekodi ya Afrika ya mbio za mita 100 ya sekunde 9.77.

Mojawapo ya malengo yake ya mwaka 2023 ni kutawala mbio za 100m kwenye Riadha za Dunia mwezi Agosti mjini Budapest, Hungary.

Alihifadhi taji lake la Kip Keino Basic Continental Tour mjini Nairobi mnamo Mei 13 alipoandikisha muda bora wa mbio za 100m mwaka huu wa sekunde 9.84.

“Niamini ninaposema kuwa sitapoteza mbio zozote za mita 100,” Omanyala ameeleza wanahabari mjini Miramas.

Omanyala aliwasili Ufaransa wikendi iliyopita na kuzuru eneo la Saint-Chamas siku ya Jumatatu na Istres hapo Jumatano kwa mazoezi, akipiga picha na mashabiki na pia kuwaandikia sahihi halisi yake.

Amefanya mazoezi ukumbini Miramas siku ya Alhamisi.

“Nafurahia sana kurejea hapa Miramas. Tumekuwa na uhusiano mzuri ninaoamini utakuwa wa muda mrefu. Ni kambi nzuri ya kujiandaa kwa michezo ya Olimpiki itakayofanyika 2024,” amesema Omanyala.

Ameongeza, “Napenda mchezo huu kwa sababu ya kufanya vijana wavutiwe nao, kufanya vijana watambue na kuelewa mchezo huu na kuwashauri kuwa si kitu kinachokuja kwa urahisi. Lazima ufanye mazoezi iwapo unataka kuwa mwanariadha wa kulipwa. Kile ninapenda sana ni kupatia vizazi vijavyo motisha ya kufanya bora kila wakati katika maisha yao.”

Omanyala alipanga kutumia muda wake na wanariadha chipukizi mjini Miramas mnamo Alhamisi alasiri.

Atahudhuria kikao na wanafunzi wa Chuo cha Chamus mjini Miramas hapo kesho Ijumaa kabla ya kuelekea mjini Rabat.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Latest Articles