Kusamehe ni uhodari na ushujaa mkubwa – Taifa Leo


DINI: Kusamehe ni uhodari na ushujaa mkubwa

DINI: Kusamehe ni uhodari na ushujaa mkubwa

NA PADRE FAUSTINE KAMUGISHA

KUSAMEHE ni ushujaa.

“Walio dhaifu hawawezi kusamehe kamwe. Msamaha ni sifa ya wenye nguvu,” alisema Mahatma Gandhi.

Kutosamehe ni unyonge. Kutosamehe ni woga. Kutosamehe ni hofu.

Kusamehe ni ujasiri. Kusamehe ni uhodari.

Dunia ina mashujaa wa msamaha wa kuigwa. Tutaja wachache. Bwana Nelson Mandela ni shujaa wa msamaha. Alikuwa na haya ya kusema kuhusu waliomtendea ubaya – “Nilivyotembea kutoka mlangoni na kuelekea lango ambalo nilikuwa natokea na kuenda kwenye uhuru wangu, nilijua kuwa kama nisingeacha ukali wangu na chuki nyuma yangu, ningeendelea kuwa gerezani, gereza la chuki.” Bwana Nelson Mandela aliwasamehe waliomfunga kwa miaka ishirini na saba.

Bwana wetu Yesu Kristu ni shujaa wa msamaha. Alipokuwa ametundikwa msalabani alisema maneno saba. Neno lake la kwanza ni, “Baba, uwasamehe kwa maana hawajui wanalofanya” (Lk 23:34).

“Seneca anatwambia kuwa watu waliosulubiwa msalabani walilaani siku yao ya kuzaliwa, wasulubishaji, mama zao na hata waliwatemea mate waliowatazama. Cicero anatwambia kuwa wakati mwingine ilikuwa lazima kukata ndimi za wale waliotundikwa msalabani ili kunyamazisha kufuru za ajabu,” aliandika Askofu Fulton Sheen katika kitabu chake, The Seven Final Phrases.

Yesu aliwasamehe waliomtemea mate. Aliwasamehe waliompiga mijeledi. Alimsamehe Pilato aliyetumia vibaya madaraka yake kutomtendea haki. Aliwasamehe waliompigilia misumari msalabani. Watu walikuwa wanamwambia Pilato, “Msulubishe, lakini yeye alipaza sauti yake, ‘Baba, uwasamehe kwa maana hawajui wanalofanya.’

Alikuwa ananing’inia kwenye misumari ya kikatili lakini hakupoteza uungwana wake. Alikuwa anawaombea msamaha waliomtendea mambo yenye sura mbaya. Aliwaombea maadui wake. Huu ni ushujaa.

Mt Josephina Bakhita (1869 – 1947) ni shujaa wa msamaha. Alizaliwa katika kijiji cha Daju Olgossa huko Darfur. Alikamatwa Sudan na kuuzwa Italia kama mtumwa.

Alisema, “Kama ningekutana na wafanyabiashara wa watumwa walionikamata na wale walionitesa, ningepiga magoti na kubusu mikono yao kwa vile, kama isingekuwa kwa sababu yao nisingekuwa mkristu na mtawa.” Aliwasamehe na wale waliomchanja chale 114 kwenye matiti, tumboni na kwenye mkono wake wa kulia.

 

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Latest Articles